Wednesday, 3 January 2024

DHANA YA HIJRA KIISLAMU NA UELEWA WA MAKUNDI YA KIGAIDI



 

 

MAKALA katika ulimwengu huu kuna Imani za dini mbalimbali ambazo kila mmoja yupo huru kuamini imani yake kwa mujibu wa mafundisho ya dini anayoiamini. Hata hivyo kuna dhana mbalimbali ambazo baadhi waumini wanazitumia katika kufanya upotoshaji kwa faida na malengo yao.

Makala hii ya leo itaangazia miongoni mwa dhana ambazo zinazotumika kinyume na ukweli wake na kuchafuliwa na makundi mbalimbali yanayofanya matendo ya kihalifu yakiwemo makundi ya kigaidi, dhana hiyo ni ya "Hijra" ambayo imechukua nafasi kubwa katika Uislamu, ambapo inaashiria tukio la kihistoria la kutangaza mageuzi makubwa katika dini ya kiislamu na kuanza awamu mpya katika historia ya kiislamu.

Hijra iliyofanywa na Mtume Mohammed (S.A.W) ni tukio la kihistoria lililotenga enzi za kujificha na kuwalingania watu kwa siri na kufanyiwa matusi ya kila aina na kuanza enzi ya kutangaza dini na kuanzisha dola imara yenye nguzo yakujivunia na kuwa na nguvu ya kujitetea, pamoja na kupanua eneo la dola ili kuvutia umma kujiunga na dini hiyo mpaka dini yenyewe ikawa nguvu na imara.

Hijra katika sharia na historia ya kiislamu ni tukio la kihistoria la Mtume (S.A.W) ambalo ni muhimu kabisa wa waislamu wote ulimwenguni. Tukio hilo limeleta mabadiliko makubwa na likapelekea mabadiliko na maendeleo katika jamii ya waislamu ulimwenguni. Waislamu wanatakiwa kutafakari kwa umakini mafunzo ya tukio hilo na kuangalia taratibu alizozichukuwa Mtume (S.A.W.) na msimamo wa maswahaba wake watukufu (R.A.) kumuunga mkono na kumsaidia kwa ajili ya kufanikisha Hijra kwa mujibu wa maamrisho ya Mwenyezi Mungu (S.W).

Lile tukio la Hijra kimekusanya mafunzo mengi ambayo Makala moja au zaidi haitoshi kuyaelezea. Lakini tunayotaka kuyabainisha hapa ni baadhi tu kati ya mafunzo na mawaidha yaliyotolewa. La kusikitisha mno kuwa baadhi ya waislamu wakitumia mafunzo hayo kinyume na ilivyoelekezwa.

Kwa ujumla, Hijra ya Mtume (S.A.W.) japokuwa ilitokea Miaka 1440, lakini atakae tia amani na kukumbuka mazingira ya tukio na hilo na taratibu zake hatapata shida.

Ilihali, akiangalia na kuchambua historia hiyo, upata ufumbuzi na suluhisho kwa matatizo yake na changamoto zake zote. Kwahiyo tunaona kwamba kupanga na kujiandaa vizuri wakati wa kumtegemea Mwenyezi Mungu (S.W) na kumtii ndivyo msingi muhimu wa kumsaidia mtu kufikia malengo yake. Hilo ndilo funzo la kwanza tunalopaswa kulielewa.

Tukiangalia maana ya hadithi hii tunapata kufahamu hekima muhimu kabisa ndiyo kwamba muislamu japokuwa anatakiwa kumtegemea na kumtii Mwenyezi Mungu (S.W) lakini anatakiwa kujipanga na kutafakari vizuri ili aipate pepo njema. Lakini baadhi ya Makundi ya Kigaidi wamekuwa wakiitumia dhana ya "Hijra" katika tafsiri tofauti kwa lengo la kuwapotosha waislamu ambao hawakupata kuifahamu dini kwa undani zaidi.

Makundi ya kigaidi yamezoea kubadilisha dhana na kupotosha maana na kugeuza ukweli kuwa batili na lililoko sahihi liwe kosa na kinyume, kwa kutumia mbinu mbalimbali zinazokusudia kudanganya vijana na kuzishawishi akili zao. Kuhusu dhana ya "Hijra" makundi ya kigaidi yanadai kuwa hijra ni wajibu na faradhi juu ya kila muislamu na kwamba Hijra huwa kwa nchi ya kiislamu ambayo kwa mtizamo wao ni ile nchi inayodhibitiwa na wao wakishikilia kauli yake Mtume (S.A.W.) "Hakika Hijra haitakatika endapo makafiri wanapiganiwa" na kauli yake (S.A.W.) iliyopokelewa na Mua'wiya anasema "Hakika Hijra haitakatika mpaka taiba ikatike na taiba haitakatika mpaka jua likuche kutoka upande wa magharibi".

Pia wenye fikra hizo wanatumia Qur'an kwa kuunga mkono mtizamo huo, ambapo wanadhani kuwa agizo la Mwenyezi Mungu (S.W.) kwa waja wake kuhama ni kwa jumla na linajumuisha hali zote kwa mujibu wa kauli ya Mwenye Mungu (S.W.).

Aya nyingine inayotumika na makundi ya kigaidi kupotosha watu wasiyokuwa na elimu ya dini ili kuthibitisha uwajibu wa Hijra ni kauli ya Mwenyezi Mungu (S.W.) "na mwenye kuhama katika njia ya Mwenyezi Mungu atapata pengi duniani pa kukimbilia, na hatapata wasaa. Na anayetoka nyumbani kwake kuhama kwa ajili ya mwenyezi Mungu na Mtume wake, kasha yakamfika mauti njiani basi umethibiti ujira wake kwa Mwenyezi mungu na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kurehemu" (Al - Nisaa: 100).

Kimsingi makundi ya kigaidi yamekuwa yakitumia yakifanya upotoshaji kutumia Aya hizo, pasipo imani na utulivu wa akili na kama hukupata elimu ya dini vizuri, vijana wengi wamekuwa wakirubuniwa kwenda Hijra pasipo kujuwa kuwa wanakwenda kutumika kutekeleza malengo ya kisiasa na kihalifu kwa vikundi vya kigaidi.

Dhana ya Hijra ina maana na matumizi tofauti na uelewa wa makundi ya kigaidi na kwamba makusudi ya Hijra katika sharia za kiislamu ni kuhama kwa ajili ya kuinusuru dini na kujilinda kutokana na fitina kutoka ardhi isiyofaa kwenda ardhi au nchi yenye amani na utulivu na kuwezesha mtu kukimu maisha yake katika mazingira mazuri na si kutafuta dola ya kiislamu na kuuwa watu wasiokuwa na hatia.

No comments:

Post a Comment

MSAMAHA NA DHANA ZAKE

    Ndugu wasomaji karibuni katika Makala yetu ya leo ambayo inahusu jambo muhimu na msingi wa uwepo wa amani na utulivu katika maisha yetu...