Tuesday, 12 December 2023

FAIDA YA KUDHIBITI HASIRA

 


 

Wapendwa wasomaji wangu, karibuni katika Makala yetu ya leo ikizungumzia mada ya hasira Hasira ni hali inayompata binadamu au mnyama mbele ya kipingamizi na katika hali hiyo mtu hughadhibika, hukwazika, kuchukia na hata kupata kitu ambacho yeye muhusika hapendi kuwa nacho.

Madhara ya uwepo kwa hasira hasa ya mara kwa mara inaweza kusababisha kuwepo kwa matendo maovu na ya kikatili ikiwemo mauaji, uharibifu wa mali ambayo yatakuwa na athari kwake, jamii na Taifa kwa ujumla.

Ili kuepuka kadhia hiyo kuna njia sahihi ya kukwepa hasira kwa mtu inayompata mara kwa mara hivyo mara nyingi anashauriwa ajaribu kuepuka vitu au mambo yanayoweza kumpelekea kumuudhi kwa mfano kuepuka kujibizana itamsaidia kuepuka ugomvi dhidi ya watu wengine.

Pia ni vyema kuepuka kuendelea kumuudhi mtu mwingine pale unapoona kuwa jambo au kitu unachomfanyia kinamkwaza maana kitendo cha kuendelea kufanya hivyo kinaweza kusababisha kutokea kwa athari na madhara makubwa.

Siku zote kitendo cha kutodhibiti hasira ni kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu kwa dini zote sababu amehimiza kuepuka hasira maana matendo yatokanayo na hasira husababisha ukatili na uovu mkubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla, vilevile hasira husababisha matatizo makubwa ya milele hapa duniani na akhera.

Kisayansi kudhibiti hasira ni muhimu kwa sababu kunasaidia kuepuka athari zifuatazo ambapo mtu mwenye hasira inampelekea kupunguza uwezo wa kufikiria kutokana na ubongo kuathirika hivyo hupoteza kumbukumbu na kupelekea kufanya matendo mabaya, hasira inaweza kusababisha kupata tatizo la moyo, vidonda vya tumbo, vile vile hasira inasababisha tatizo la kupungua kwa kinga ya mwili.

 

Kwa upande wa mwanamke inasababisha kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi sababu kuu ni kutokea kwa mabadiliko ya mzunguko wa homoni na hata wakati mwengine hasira kupelekea kuharibika kwa ujauzito.

Ili kuepuka kuwa na hasira inatakiwa yafanyike mambo yafuatayo. Kwanza kujua sababu ya kuwa na hasira zako kwa maana ya nini kinapelekea, pili kujua na kukwepa sababu za hasira ulizonazo, tatu kujizuia kuchukua hatua na kufanya jambo lolote baya pale unapopatwa na hasira, wakati mwingine kitaalamu unashauriwa uhesabu hadi ishirini ili ujipe muda wa kuchukua maamuzi yako yanayotokana na hasira uliyonayo na kama kuhesabu anzia 20 kwenda 1.

Vile vile ili kumaliza hasira jitahidi kufanya kitu au jambo lingine mbadala, jitahidi kukaa kimya ili kuzuia kuongezeka kwa hasira, ondoka eneo au mazingira ambayo yamekupelekea au kusababisha hasira, badili mada na aina ya mazungumzo pamoja na mtu ambaye amekusababishia upate hasira. Jambo la kuzingatia ni kuwa suala la kuwa na hasira halishabihiani na hali mtu, uwezo wake, elimu yake, dini, kabila, rangi, umri, jinsi na hata cheo chake.

Hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kuhakikisha kuwa anaheshimu mipaka ya ubinadamu na utu kwa mwengine ili kuzuia kusababisha kutokea kwa sababu ya kupata hasira. Waswahili wanasema heri lawama kuliko fedheha wakimaanisha ni bora ukakubali kujishusha na kuwa mpole ili kuepuka kusababisha hasira kuliko kutaka kujibizana ambapo hali itapelekea kushikwa kwa hasira na kufanya maamuzi ya hatari yenye hasara kwako, jamii na Taifa kwa ujumla kwa maana nyingine ni kuwa (hasira hasara).

Wito wangu ni vyema kila mmoja kuhakikisha anadhibiti hasira zake pindi anapopatwa na jambo au kitu kinachomkwaza au kumuudhi, katika hatua hii kuna baadhi ya watu wenye mlengo wa kupotosha watu wengine wanaweza pia kutumia maneno au kufanya vitendo vya uchonganishi dhidi ya dini nyingine, Serikali au jamii nyingine ili kuwakwaza na kuwaudhi wengine kwa lengo la kuwasababishia hasira itakayowapelekea kufanya vitendo vya kihalifu dhidi ya makundi hayo wanayochonganishwa nayo.

Hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kusoma alama za nyakati ili kuweza kubaini lengo la mtu anayekusababishia hasira, kufanya hivyo itasaidia kuwa na uwezo wa kukwepa sababu za kupata hasira. Tuendelee kudhibiti hasira zetu ili kuendelea kulinda amani na utulivu katika jamii na Nchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

MSAMAHA NA DHANA ZAKE

    Ndugu wasomaji karibuni katika Makala yetu ya leo ambayo inahusu jambo muhimu na msingi wa uwepo wa amani na utulivu katika maisha yetu...