MWENYEZI Mungu (S.W) amemtuma Mtume wake Muhammad (S.A.W.) kwa ajili ya rehma kwa walimwengu wote, ambapo Mwenyezi Mungu (S.W) amesema "Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote" Surat Al - Anbiyaa, aya 107 aya hii inatufundisha kuwa ujio wa Mtume Muhammad (SAW) ni rehema ya Mungu kwa viumbe wote waislamu na wasio waislamu, waarabu na wasio waarabu kwani mafundisho yake yangefuatishwa duni ingekuwa mahala pa amani.
Mafundisho ya dini ya kiislam yanawataka Waislam wawe na huruma kwa binaadamu wote waliopo duniani, Mtume Muhammad (S.A.W) amesisitiza maana hiyo kwa kusema "Hakika Mwenyezi Mungu hawahurumii wasiowahurumia wanandamu wenzao"hadithi hii ya mtume haikusema waislamu wenzo pekee bali imeongelea binaadamu kwa jumla.
Hivyo, Wanadamu wote wanatakiwa kuhurumiana bila kujali itikadi ya dini zao, kabila wala rangi, ambapo moja wapo ya misingi ya tabia njema katika dini ya kiislamu ni kuwaonea huruma wasio Waislamu na kuwatendea wema muda wakua hawajawafanyia uadui waislamu ama vitendo viovu.
Tukizisoma aya za Qur.ni ama kufuatilia hadithi za Mtume Muhammad (SAW) TUTATAMBU KUWA, huruma katika Uislamu ni jambo la viumbe wote, siyo kwa watu maalumu wala kwa baadhi ya Viumbe tu. Mtume Muhammad (S.A.W) amesema; "Kwa kweli Mwenyezi Mungu hamuhurumii ila aliye wahurumia wengine, Maswahaba wakasema; Ewe Mtume! Sote hivyo kwa maana tunawahurumia wengine. Mtume akasema, sikusudii mnavyofanya na wenzenu, bali na wanadamu wote".
Hivyo, alama ya kwanza ya kupambika na tabia nzuri katika mfumo wa maadili mema ya kiislam ni kuwahurumia viumbe wote hadi wanyama na si binadamu peke yao tunajifunza hilo katika mafundisho mema ya dini ya kiislamu.
Mtume Muhammad (S.A.W) amesema kuwa "aliadhibiwa mwanamke kwa ajili ya kumtesa Paka aliyemfungia ndani hakumpa chakula wala hakumuachia ajitafutie mwenyewe chakula, jambo hilo likasababisha aingie motoni". Katika hadithi hii tunajifunza jinsi huruma ilivyokuwa muhimu kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya kiislam.
Mtume alikuwa ni mfano bora wa huruma kwa viumbe wote hata wanyama, katika maelekezo kwa umma huu anasema ( Hakika Allah ameagiza kufanya wema katika kila kitu hivyo hata mkichinja wanyama kwa ajili ya chakula wachinjeni vizuri ) na katika hadihi nyengine anasema ( mmoja wenu akimchinja mnyama anoe kisu chake vizuri na amlaze vizuri mnyama anayemchinja ili afanye jambo hilo kwa haraka).
Hadithi iliyotangulia inaelekeza huruma hata katika vitu vya machungu, sote tunajua kuwa, ng'mbe, mbuzi, kuku na wanyama wengine wanaoliwa kitendo cha kuwachinja ni kitendo cha maimivu kinacho sitisha uhai wao ili watumiwe kuwa ni kitoweo, hata hivyo bado Mtume anahimiza kuwa zoezi hilo lifanywe kwa huruma kisu kinolewe vizuri ili mnyama asiwe kwenye maumivu muda mrefu,
Mfano mwingine ni maelekezo aliyoyatoa mtume Muhammad kuhusu kukataza kuwatukana wafuasi wa dini nyengine wanaoishi katika miji ya waoslamu kwa makubaliano, pale aliposema "atakemtukana mfuasi wa dini nyengine anaekaa katika miji ya kiislamu kwa makubaliano ya Amani (dhimmyyu) zitampata laana za Mwenyezimungu" maelekezo haya yanahimiza kuwatendea maadili mema watu wa Imani nyengine.
Tukiangalia dhana iliyojengeka na baadhi ya wanaharakati wa kiislamu nchini Tanzania ni kuwa asiye muislamu hana haki ya kuishi, kuheshimiwa ama kuhurumiwa uelewa huu ni kinyume na mafundisho ya dini ya kiislamu, kwani rejea zote hapo juu zinaeleza kuwa waislamu wanatakiwa kukaa kwa wema na watu wote bila kujali dini zao na itikadi zao.
Kwa nchi kama Tanzania ambapo kuna idadi inayokaribiana ya waumini wa dini mbili mafunzo haya ya dini ya kiislamu ni wajibu kutekelezwa kutoka pande zote ili jamii ya watanzania iendelee kuishi kwa utulivu na Amani ili kujenga jamii salama inayopendana, hii itasaidia kuto wapa nafasi baadhi ya watu wenye nia ya kuwagombanisha watanzania kwa kigezo cha dini.
Ni matarajio yangu kuwa, kila muislamu nchini Tanzania na kwengine duniani atakae soma Makala hii atakuwa na huruma kwa waislamu wenzake na jamii yake bila kujali Imani na itikadi ya jamii hiyo ili awe ni kioo kwa jamii inayomzunguka tukiishi hivi maovu na uhalifu katika jamii utaisha na kufanya jamii iishi kwenye upendo na maelewano.

No comments:
Post a Comment