Wednesday, 15 November 2023

AMANI NA USALAMA KATIKA MTAZAMO WA UISLAMU


 

Dini ya Uislamu ina mitazamo inayofanana na dini nyingine za mbinguni kuhusu suala hili la amani na usalama. Katika mtazamo wa Uislamu usalama una maana ya amani na utulivu katika jamii. Katika upande mwingine, usalama na minyambuliko yake ni neno lililotumiwa mara nyingi katika aya za Qur'ani tukufu. Neno hilo na amani kwa ujumla limezungumziwa katika karibu aya 140 za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Katika mtazamo wa Uislamu, usalama na Uislamu ni maneno mawili yanayoambatana, yenye mfungamano na yasiyotengana. Wasomi wa Kiislamu wanasisitiza kuwa, maneno mawili yana maana ya amani na usalama:

 

 

AMANI KATIKA UISLAMU

Kwanza ni neno "Silm" au "Al Salm" ambalo katika lugha ya Kiarabu lina maana ya utulivu, kusalimika au usalama kwa istilahi ya zama hizi. Usalama na amani vina mfungamano na Mwenyezi Mungu Muumba. Mwenyezi Muumba mwenyewe amejitaja kuwa ni "Assalam" kwa maana ya amani na Mwenye amani na salama na kwa msingi huo kila usalama na amani ni mwangwi wa dhati yake tukufu. Dhati ya mwanadamu pia daima huwa katika hali ya kustawi na kufanya harakati za kuelekea kwenye amani na utulivu kamili ambao haupatikana ila kwa amani na usalama mutlaki, yaani dhati ya Mwenyezi Mungu Muumba. Hii ndiyo siri ya falsafa ya wito wa Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu ambayo daima humlingania mwanadamu wito wa amani na usalama na kumuelekeza kwenye amani na usalama mutlaki na kamili. Aya ya 208 ya Suratul Baqara inasema:

 

یَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُواْ ادْخُلُواْ فِی السِّلْمِ کَافَّةً وَلاَ تَتَّبِعُواْ خُطُوَاتِ الشَّیْطَانِ إِنَّهُ لَکُمْ عَدُوٌّ مُّبِینٌ

 

Enyi Mlioamini! Ingieni katika usalama nyote. Wala msifuate nyayo za She'tani; hakika yeye kwenu ni adui aliyewazi.

 

Vilevile aya ya 61 ya Suratul Anfal inasema:

 

وَإِن جَنَحُواْ لِلسَّلْمِ فَاجْنَحْ لَهَا وَتَوَکَّلْ عَلَى اللَّهِ إِنَّهُ هُوَ السَّمِیعُ الْعَلِیمُ

 

Na (wapinzani wako) wakielekea kwenye amani nawe pia elekea, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.

 

Neno "Islam" pia linatokana na msingi wa neno "Silm", na kwa hakika lina maana ya kumfuata Mwenyezi Mungu ambaye Yeye mwenyewe ndiye amani na usalama mutlaki na utulivu kamili.

 

Neno jingine ni "sulh" ambalo lina maana na amani, maelewano na uhusiano mwema baina ya wanadamu. Uislamu umetumia neno hilo ukitaka kuwepo upendo, kuheshimiana, kujiepusha na uchokozi na uhasama na kuchupa mipaka ya wanadamu wengine.

 

Ili kuweza kupatikana amani na uadilifu, Uislamu umeweka safari yenye awamu tatu tofauti

1.   Usalama na amani ya ndani ya nafsi

2.  Amani na usalama katika Uislamu ni amani na usalama wa jamii.

3.    Amani na usalama inahusiana na usalama na amani kwa wasio Waislamu.   Miongoni mwa misingi na kanuni zinazotawala jamii ya Kiislamu ni kuishi kwa amani na usalama na wasio Waislamu. Kinyume na fikra na dhana za wanafikra wengi wasio Waislamu na propaganda chafu za nchi za Magharibi, Uislamu ni dini ya amani na kuishi kwa usalama na wasio Waislamu. Hii ni pamoja na kwamba, huwezi kupata hata aya moja ya Qur'ani inayowalazimisha watu kukubali dini hiyo kwa vita na mabavu.

No comments:

Post a Comment

MSAMAHA NA DHANA ZAKE

    Ndugu wasomaji karibuni katika Makala yetu ya leo ambayo inahusu jambo muhimu na msingi wa uwepo wa amani na utulivu katika maisha yetu...