Ndugu wasomaji karibuni katika
Makala yetu ya leo ambayo inahusu jambo muhimu na msingi wa uwepo wa amani na
utulivu katika maisha yetu ya kila siku. Mada hii ya msamaha ni muhimu kwa
sababu inahusisha hisia za mtu moja kwa moja katika kufanya maamuzi baada ya
kukosewa au kukosea.
Neno Msamaha linatafsiriwa kwa dhana mbalimbali kama ni uamuzi wa Mwenyezi Mungu au mtu mwingine wa kuamua kutofuatilia matendo na makosa ambayo ametendewa na mtu mwingine.
Katika Luka 6:37 imeelezwa kuwa maana ya msamaha ni "kuachilia". achilieni nanyi mtaachiliwa.
Katika Quraani Surat taghabun aya ya 14 imeeleza maana ya neno msamaha na hatua zake ambapo imefafanuliwa kuwa msamaha au kuwia radhi ni hali ya kutotilia mkazo au maanani kosa lililofanyika hii kwa mujibu wa Imamu Ali (A). Msamaha ni taji la sifa kwa muungwana. Pia katika aya hii imeeleza kuwa msamaha ni uvumilivu ambao unazuia kuadhibu kwa maneno au vitendo, kadhalika msamaha ni kufuta kile kitendo kilichofanywa na kuondoa dhana ya matokeo hasi ambayo yametokana na kufanyiwa makosa.
Vile vile tafsiri hii ya neno kabisa cha neno kisasi kupatana na aliyekiri msamaha inazidi kueleza kuwa ni kinyume lakini ni tofauti na neno kusahau, kutetea au makosa. Hii ina maana kuwa mtu anaweza akakusamehe ila bado akawa hajasahau lile jambo au tukio alilotendewa na mtu aliyemkosea.
Kwa upande wa dini zote unasisitiza na kuhimiza watu kusamehe pindi wanapokosewa, hali hiyo ya kusamehe inaleta nguvu hasa kwa mtu anayetoa msamaha na nafuu hiyo inaweza kuenea kuanzia katika nafsi ya mtoaji msamaha hadi mwilini kwake kote.
Msamaha siku zote unajumuisha mambo matatu ambayo ni msamaha wenyewe, uvumilivu na kuachiliwa.
Chanzo kikuu cha msamaha kilianza pale dhambi na makosa yalipoanza maana pasipo na dhambi na makosa msamaha usingekuwepo. Hivyo msamaha upo maalumu kwa ajili ya wale binadamu ambao ni watenda dhambi na wafanya makosa.
Kwahiyo, tambua kwenye dhambi na makosa hapo ndipo penye msamaha. Kuomba msamaha ni roho na mtu ambaye atagoma kuomba msamaha basi huyo ana roho ya kishetani maana naye aligoma kuomba msamaha pindi alipomkosea Mwenyezi Mungu na Shetani kuahidi kuwa atawapoteza na waja wengine.
Ili uwe mtu mwenye uwezo wa kutoa msamaha dhidi ya aliyekukosea lazima uwe na sifa zifuatazo.
Uwe mtu mwenye huruma, mtu mwenye uvumilivu, mtu mwenye upendo dhidi ya wengine, lazima uwe mtu uliye na hofu ya Mwenyezi Mungu pamoja na kumjua Mwenyezi Mungu na kwamba Mungu yeye ndiye aliyeanzisha msamaha kwa wanaomkosea mwisho mtu mwenye uwezo wa kutoa msamaha huwa ambaye anajua umuhimu wa msamaha pindi anapokosewa.
Je, utatambuaje au dalili na ishara za mtu aliyekusamehe baada ya kumkosea.
Hawezi kukuzungumzia vibaya mbele ya watu wengine, atakuchangamkia tena kama ilivyokuwa kabla ya kukoseana, endapo utapatwa au utakuwa na shida au tatizo hatosita kukusaidia na atakusaidia bila kinyongo chochote, pia mtu aliyekusamehe atakuwa anakusalimia na kupokea salamu zako pindi unapomsalimia kama ilivyokuwa zamani.
Vile vile katika tendo zima la msamaha mtu anayekusamehe anaweza kufanya hivyo bila kumuomba msamaha ila kama itatakiwa aliyekosea mpaka aombe msamaha yeye kuna mambo muhimu ya kuzingatia ambayo ni:-
Afahamu na kujua njia sahihi ya kuomba msamaha ikiwa hata kulia au kupiga magoti ili amridhishe anayemuomba msamaha, mwombaji msamaha afahamu umuhimu wa kuomba msamaha juu ya lile kosa alilotenda, ajue njia sahihi na namna ya kuacha kutorudia kosa alilotenda awali, mwisho na kwa umuhimu awe na imani kuwa Mwenyezi Mungu amehimiza kuomba msamaha pale tunapokoseana.
Wito wangu ni kuwa makosa kwa maumbile ya mwanadamu ni jambo la kawaida ingawa anaweza kukosea bahati mbaya ama makusudi. Hata hivyo kwa hali yoyote ile bado haizuii kwa mtu aliyekosea kusamehewa kwa kosa alilotenda. Siku zote msamaha huleta furaha na amani ya moyo hii itasaidia kupata jamii na Taifa lenye upendo, utulivu na amani ambapo itasukuma uwepo wa maendeleo kwa vizazi husika.


.png)



.png)